Leviticus 9:2-22

2 aAkamwambia Aroni, “Chukua ndama dume kwa ajili ya sadaka yako ya dhambi, na kondoo dume kwa sadaka yako ya kuteketezwa, wote wawili wasiwe na dosari, nao uwalete mbele za Bwana. 3 bKisha waambie Waisraeli: ‘Chukueni mbuzi dume kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na ndama na mwana-kondoo, wote wawili wawe wa umri wa mwaka mmoja, na wasio na dosari, kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, 4 cna pia maksai na kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya amani, ili kutoa dhabihu mbele za Bwana, pamoja na sadaka ya nafaka iliyochanganywa na mafuta. Kwa kuwa leo Bwana atawatokea.’ ”

5Wakavileta vile vitu Mose alivyowaagiza mbele ya Hema la Kukutania, nalo kusanyiko lote likakaribia na kusimama mbele za Bwana. 6Ndipo Mose akasema, “Hili ndilo Bwana alilowaagiza mlifanye, ili utukufu wa Bwana upate kuonekana kwenu.”

7 dMose akamwambia Aroni, “Njoo madhabahuni ili utoe dhabihu yako ya sadaka ya dhambi na sadaka yako ya kuteketezwa, ufanye upatanisho kwa ajili yako mwenyewe na kwa ajili ya watu. Kisha utoe sadaka ya upatanisho kwa ajili ya watu, kama vile Bwana alivyoagiza.”

8 eHivyo Aroni akaja madhabahuni na kumchinja yule ndama kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili yake mwenyewe. 9Wanawe wakamletea damu, naye akachovya kidole chake katika hiyo damu, akaitia kwenye pembe za madhabahu, nayo damu iliyobaki akaimwaga chini ya madhabahu. 10Juu ya madhabahu akateketeza mafuta, figo na mafuta yanayofunika ini kutoka kwenye hiyo sadaka ya dhambi, kama Bwana alivyomwagiza Mose. 11 fAkateketeza nyama na ngozi nje ya kambi.

12 gKisha Aroni akachinja sadaka ya kuteketezwa. Wanawe wakamletea damu, naye akainyunyiza pande zote za madhabahu. 13 hWakamletea sadaka ya kuteketezwa kipande kwa kipande, pamoja na kichwa, naye akaviteketeza juu ya madhabahu. 14 iAkasafisha sehemu za ndani na miguu, akaviteketeza juu ya sadaka ya kuteketezwa juu ya madhabahu.

15 jKisha Aroni akaleta sadaka ile iliyokuwa kwa ajili ya watu. Akachukua yule mbuzi wa sadaka ya dhambi kwa ajili ya watu, akamchinja na kumtoa kwa ajili ya sadaka ya dhambi, kama alivyofanya kwa ile ya kwanza.

16 kAroni akaleta sadaka ya kuteketezwa na kuitoa kama ilivyoelekezwa. 17 lPia akaleta sadaka ya nafaka, akachukua konzi moja na kuiteketeza juu ya madhabahu, pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya asubuhi.

18Akachinja maksai na kondoo dume kama sadaka ya amani kwa ajili ya watu. Wanawe Aroni wakampa ile damu, naye akainyunyiza kwenye madhabahu pande zote. 19Lakini sehemu zile za mafuta ya yule maksai na kondoo dume, yaani mafuta ya mkia, mafuta yaliyofunika tumbo, ya figo na yaliyofunika ini, 20hivi vyote wakaviweka juu ya vidari, kisha Aroni akayateketeza hayo mafuta ya wanyama juu ya madhabahu. 21 mAroni akaviinua vile vidari na paja la kulia mbele za Bwana ili viwe sadaka ya kuinuliwa, kama Mose alivyoagiza.

22 nKisha Aroni akainua mikono yake kuwaelekea watu na kuwabariki. Naye baada ya kutoa dhabihu ya sadaka ya dhambi, sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya amani, akashuka chini.

Copyright information for SwhNEN